Psalms 19

Utukufu Wa Mungu Katika Uumbaji

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi)


1 aMbingu zinatangaza utukufu wa Mungu,
anga zahubiri kazi ya mikono yake.

2 bSiku baada ya siku zinatoa habari,
usiku baada ya usiku zinatangaza maarifa.

3 Hakuna msemo wala lugha,
ambapo sauti zao hazisikiki.

4 cSauti yao imeenea duniani pote,
nayo maneno yao yameenea
hadi miisho ya ulimwengu.

Katika mbingu amepiga hema kwa ajili ya jua,

5 dlinafanana na bwana arusi
akitoka chumbani mwake,
kama shujaa afurahiavyo
kukamilisha kushindana kwake.

6 eHuchomoza upande mmoja wa mbingu,
na kufanya mzunguko wake
hadi upande mwingine.
Hakuna kilichojificha joto lake.


7 fSheria ya Bwana ni kamilifu,
ikihuisha nafsi.
Shuhuda za Bwana ni za kuaminika,
zikimpa mjinga hekima.

8 gMaagizo ya Bwana ni kamili,
nayo hufurahisha moyo.
Amri za Bwana huangaza,
zatia nuru machoni.

9 hKumcha Bwana ni utakatifu,
nako kwadumu milele.
Amri za Bwana ni za hakika,
nazo zina haki.

10 iNi za thamani kuliko dhahabu,
kuliko dhahabu iliyo safi sana,
ni tamu kuliko asali,
kuliko asali kutoka kwenye sega.

11 jKwa hizo mtumishi wako anaonywa,
katika kuzishika kuna thawabu kubwa.


12 kNi nani awezaye kutambua makosa yake?
Nisamehe makosa yangu nisiyoyajua.

13 lMlinde mtumishi wako na dhambi za makusudi,
nazo zisinitawale.
Ndipo nitakapokuwa sina lawama,
wala sitakuwa na hatia ya kosa kubwa.


14 mManeno ya kinywa changu
na mawazo ya moyo wangu,
yapate kibali mbele zako, Ee Bwana,
Mwamba wangu na Mkombozi wangu.
Copyright information for SwhKC